SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limemteua Kocha wa Singida Black Stars, Miguel Angel Gamondi raia wa Argentina kuwa Kaimu kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' akichukua mikoba ya Hemed Suleiman 'Morocco' ambaye mkataba wake umesitishwa kwa makubaliano ya pande mbili.
Taarifa ya leo Novemba 4, 2025 iliyotolewa na TFF imeeleza kuwa mazungumzo yameshafanyika kati ya TFF na Singida Black Stars kuhusu Kocha huyo kuchukua majukumu hayo mapya na kubainisha kuwa kocha huyo wa zamani wa Young Africans Sc ataiongoza Taifa Stars kwenye Fainali za AFCON zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Desemba mwaka huu.
